Baada ya mapumziko mafupi, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wamerejea mazoezini tangu juzi wakiwa na malengo makubwa kuelekea mechi zao za mwisho za msimu huu wa 2024/25
Kikosi cha kocha Miloud Hamdi kinajiandaa kwa mechi ya mzunguko wa 27 dhidi ya Namungo FC itakayopigwa Jumanne, Mei 13 katika dimba la KMC Complex
Hamdi ameweka wazi kuwa malengo ya Yanga, kushinda kila mchezo uliosalia ili kutetea taji la Ligi Kuu na pia kuhakikisha wanatetea taji la Kombe la Shirikisho la CRDB kwa msimu wa nne mfululizo.
Ratiba ya Mechi Muhimu kwa mwezi Mei 2025
-
Mei 13: Yanga vs Namungo FC – Ligi Kuu, mzunguko wa 27
-
Mei 18: Yanga vs JKT Tanzania – Nusu fainali ya Kombe la CRDB, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga
Endapo Yanga watafanikiwa kuitupa nje JKT Tanzania, katika mchezo wa fainali wanaweza kukutana na watani wao wa jadi, Simba SC, endapo nao watawatoa Singida Black Stars katika nusu fainali.
Hii italeta fursa ya fainali kali ya watani wa jadi kwenye Kombe la CRDB, ambayo mashabiki wengi wa Yanga wanaitamani, hasa baada ya sintofahamu iliyoikumba mechi ya ligi baina ya timu hizo iliyopaswa kupigwa March 08
Sintofahamu ya Mechi ya Yanga vs Simba
Ikumbukwe kuwa, mechi namba 184 ya mzunguko wa pili ya Ligi Kuu kati ya Yanga na Simba haikuchezwa baada ya Simba 'kuingia mitini' huku Bodi ya Ligi ikiahirisha mchezo huo kuwanusuru Simba na adhabu kwa mujibu wa kanuni
Yanga imeweka ngumu ya kutocheza licha ya mchezo huo namba 184 kupangiwa tahere mpya, Juni 15
Rais wa TFF Wallace Karia jana alithibitisha kuwa bado sakata la mechi hiyo linashughulikiwa na vyombo vya kisheria na hafahamu litamalizika lini