Kocha mkuu wa Klabu ya Yanga, Miloud Hamdi, ameonesha furaha kufuatia kurejea kwa nyota waliokuwa majeruhi, kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua na mshambuliaji Kennedy Musonda, waliorejea mazoezini kuelekea ukingoni mwa msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alianza kurejea kiungo Khalid Aucho, ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa muda baada ya kupata jeraha la kuchanika misuli ya paja, kambini mwa Yanga hali imezidi kuwa na matumaini kufuatia kurejea kwa Zouzoua aliyeumia katika mechi dhidi ya Azam na Musonda aliyepata jeraha kwenye pambano la kwanza la Kombe la Muungano.
Wachezaji hao wamejiunga na wenzao katika maandalizi ya mechi za kufungia msimu, ikiwemo mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo utakaopigwa Mei 13, na nusu fainali ya Kombe la CRDB dhidi ya JKT Tanzania Mei 18.
Kocha Hamdi amesema kurejea kwa wachezaji hao kunampa uhuru zaidi wa kimkakati:
"Nafurahia kuwa na kikosi kipana ambacho kinanipa nguvu ya kufanya mzunguko navyotaka kulingana na wapinzani watakavyokuja," alisema.
Yanga, ambayo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa alama 70 baada ya mechi 26—ikishinda 23, sare moja na kupoteza miwili—inaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa kwa mara nyingine, ikihitaji kushinda mechi zote tatu zilizobaki
Mashabiki wa Yanga wanasubiri kwa hamu kuishuhudia timu yao ikiwa imekamilika katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Namungo Fc wiki ijayo baada ya kutwaa michuano ya Muungano