Mwanasheria wa zamani wa Yanga Simon Patrick amewataka Wanachama na Mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwa wavumilivu kutokana na yale ambayo klabu yao inapitia
Aidha Patrick ambaye aliondoka Yanga August 2024 baada ya uteuzi ICC, amesema maamuzi madogo yaliyofanywa na CAS yamewaumiza wengi lakini wanapaswa kuwapa moyo viongozi wao kwani wanayopitia nyuma ya pazia ni mambo makubwa
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Patrick ameandika ujumbe huu;
"Vita dhidi ya wahuni haijawahi kuwa rahisi. Wanayanga wenzangu, najua maamuzi madogo ya CAS yamewaumiza, ila tuwapongeze viongozi wetu kwa kupinga uhuni kwa vitendo na nina uhakika hawajakata tamaa.
Najua hawawezi kujitokeza kuwaeleza wanayoyapitia nyuma ya pazia, ila ipo siku mtawaelewa.
Niwaombe wana Yanga muendelea kuwapa moyo na kuwaunga mkono kwa nguvu. Kwa muda niliotumikia klabu, nimejionea jinsi ilivyo changamoto kuiongoza klabu ya Yanga.
Mwisho, nitumie fursa hii kuwaomba radhi ndugu zangu waandishi wa habari. Nimekuwa sipokei simu zenu, si kwamba sipendi kuzungumza nanyi, bali kwa sasa mimi ni mwanachama mtiifu wa Yanga, Nawaombeni mniruhusu niendelee kupumzika soka la Bongo, Yanga ina watu makini wengi na wenye weredi tuwape muda waendelee kutupambania," aliandika Simon