Msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu Tanzania Bara umeendelea kuwa wa kipekee kwa mabingwa watetezi, Young Africans, wakionyesha uimara wa kiuchezaji, maamuzi magumu ya kiuongozi, na ushupavu wa wachezaji wake – safari ambayo kwa hakika imekuwa ni ya kupindua meza kisoka
Mwanzo wa Kipekee
Yanga ilianza msimu kwa kishindo, ilitwaa Ngao ya Jamii na ikashinda mechi zote nane za mwanzo wa ligi. Kikosi kilionekana kimeiva, wachezaji walikuwa kwenye kiwango cha juu, na mashabiki walikuwa na matumaini ya msimu mwingine wa mafanikio
Hali hii ilitengeneza taswira ya timu isiyotetereka, lakini changamoto zilijitokeza haraka kuliko wengi walivyotarajia. Ni baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za ligi kuu dhidii ya Azam Fc na Tabora United
Vipigo hivyo vilipelekea uongozi kuchukua mamuzi magumu kwa kumuondoa kocha Miguel Gamondi pamoja na kuhama kutoka uwanja wa Azam Complex kama uwanja wa nyumbani na kuhamia KMC Complex
Sead Ramovic: Moto Mpya, Lakini wa Muda
Baada ya kumuondoa Gamondi, Yanga ikatangaza kumuajiri kocha Sead Ramovic ambaye alijiunga na Wananchi akitokea klabu ya TS Galaxy ambayo aliachana nayo wiki chache nyuma
Lakini Ramovic nae hakuanza vyema, katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), Yanga ilikumbana na vipigo viwili mfululizo vilivyoathiri morali ya timu. Matokeo haya hayakuwa tu pigo kwa mashabiki, bali yalionesha wazi kuwa kulikuwa na changamoto katika mbinu za uchezaji
Uongozi chini ya Rais Injinia Hersi Said wakaendelea kumuamini Ramovic licha ya presha kubwa kutoka nje kwa kuwa kocha huyo hakuwahi kupata mafanikio yoyote katika timu alizofundisha kabla
Ramovic akafanikiwa kubadili mambo ndani ya muda mfupi, aliirudishia timu ari ya kupambana na kutengeneza matumaini mapya
Chini yake, Yanga karibu kabisa ifanikishe kufuzu kwa robo fainali ya CAF CL licha ya mwanzo mbaya. Kwa muda mfupi, Ramovic alionekana kuirudisha timu katika njia sahihi – lakini safari yake ikakatizwa ghafla baada ya kupata ofa nono kutoka CR Belouizdad ya Algeria
Miloud Hamdi: Mkombozi wa Wananchi
Mara baada ya Ramovic kuondoka, kocha Miloud Hamdi akateuliwa kuiongoza Yanga. Kwa wengi, ilikuwa kama dau la majaribio – lakini Hamdi hakuhitaji muda mrefu kuonesha kuwa ni mtu sahihi kwa kazi hiyo.
Katika mechi 10 za awali, ameiongoza Yanga kwa mafanikio ya kushangaza: ameshinda 9 na kutoa sare 1, matokeo ambayo yameirudisha timu kileleni mwa msimamo.
Kwa sasa, Yanga inaongoza ligi ikiwa na alama 67, ikiwa mbele kwa alama 10 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC, ambao bado wana mechi tatu za viporo.
Zikiwa zimebaki mechi nne tu, Yanga ipo kwenye nafasi nzuri sana ya kutetea ubingwa wake kwa mara ya nne mfululizo – itakuwa rekodi nyingine ya aina yake katika historia ya klabu hiyo.
Safari ya Yanga msimu huu ni hadithi ya ujasiri, mabadiliko ya kimkakati, na kiu ya mafanikio. Kutoka kwa mwanzo mzuri, kupitia changamoto za CAF, hadi mabadiliko ya benchi la ufundi mara mbili, timu imeendelea kusimama imara
Ikiwa wachezaji wataendeleza kasi waliyoanza nayo chini ya Hamdi, basi hakuna atakayeizuia Yanga SC kuendeleza utawala wake katika soka Tanzania