Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Yanga, Clatous Chama, anaendelea kukumbwa na hali ya kutopata muda wa kutosha wa kucheza katika kikosi cha kocha Miloud Hamdi
Nyota huyo wa kimataifa kutoka Zambia, ambaye anafahamika kwa ubunifu na pasi za mwisho zenye ubora, ameonekana kutopewa nafasi katika kikosi cha kwanza kwa muda sasa
Katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union uliopigwa Aprili 7 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Chama pamoja na mshambuliaji mwenzake kutoka Zambia, Kennedy Musonda, waliingia dakika ya 83—wakicheza takribani dakika 7 tu kabla ya filimbi ya mwisho
Ushindi wa 1-0 kwa Yanga ulipatikana, lakini mashabiki walibaki na maswali mengi kuhusu kwanini Chama hakuingia mapema
Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu, Chama anaonekana kutokuwa na furaha kutokana na hali hiyo kwani alijiunga Yanga akiwa na matarajio makubwa
Akiwa na rekodi nzuri ya pasi za mabao, kufunga, na kuongoza mashambulizi, wengi wanahisi Yanga haijatumia kikamilifu kipaji chake
Mashabiki wa Yanga wameanza kutoa sauti zao mitandaoni, wakitaka kiungo huyo apewe muda zaidi uwanjani. Moja ya mashabiki aliandika kwenye X (zamani Twitter):
"Tuna wachezaji wenye ubora wa hali ya juu kama Chama, lakini hatuwatumii. Kocha Hamdi anapaswa kumwamini zaidi huyu jamaa, anabadilisha mchezo ndani ya dakika chache!," aliandika
Chama alitua Yanga akitokea Simba akiwa na hadhi ya mchezaji mkubwa na alitarajiwa kuwa sehemu ya wachezaji wa kuamua mechi
Hata hivyo nafasi yake imekuwa finyu, huku akitupwa kwenye benchi mara kwa mara. Kwa upande wa Chama, lugha ya mwili wake uwanjani na nje ya uwanja inaeleza mengi