Yanga ilipata ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Jumatatu, Aprili 7, katika Uwanja wa KMC Complex
Hata hivyo, ushindi huo uliambatana na habari mbaya baada ya kiungo wao muhimu, Khalid Aucho, kushindwa kumaliza dakika 90 kutokana na majeraha ya nyama za paja (hamstring)
Aucho ambaye amekuwa mhimili wa safu ya kiungo ya Yanga msimu huu, alitolewa mapema kutokana na jeraha hilo ambalo linatarajiwa kumuweka nje kwa wiki tatu
Meneja wa Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, alithibitisha jeraha hilo kwa kusema:
"Khalid Aucho ameumia nyama za paja wakati wa mchezo dhidi ya Coastal Union. Hatakuwepo kwenye mchezo wetu unaofuata wa ligi dhidi ya Azam FC utakaochezwa Alhamisi, Aprili 10," alisema Kamwe
Hii ni pigo kwa Yanga, hasa ikizingatiwa kuwa mechi dhidi ya Azam FC ni muhimu katika mbio za ubingwa
Aucho, raia wa Uganda, amekuwa na mchango mkubwa msimu huu kutokana na uwezo wake wa kusoma mchezo, kupokonya mipira, na kutuliza mashambulizi ya wapinzani
Kocha mkuu Miloud Hamdi atalazimika kufanya mabadiliko kwenye safu ya kiungo. Wachezaji kama Duke Abuya au Mudathir Yahya huenda wakapewa majukumu zaidi katika eneo hilo
Wakati timu ya madaktari ikiendelea na tathmini ya kina kuhusu hali yake, mashabiki wa Yanga wanatumai kuwa nyota huyo atapona haraka na kurejea uwanjani kabla ya michezo ya mwisho wa msimu