Rais wa Yanga Injinia Hersi Said akiwa sambamba na Mtendaji Mkuu Andre Mtine wamehudhuria kikao kilichoitishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh Palamagamba Kabudi kutatua mgogoro ulioibuka baada ya Bodi ya Ligi kuahirisha mchezo namba 184 ligi kuu ya NBC kati ya Yanga dhidi ya Simba uliopaswa kupigwa March 08 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Maafisa kutoka Bodi ya Ligi, TFF na klabu ya Simba nao wamehudhuria kikao hicho kinachofanyika katika ukumbi ulioko ndani ya uwanja wa Benjamin Mkapa
Hersi hakuwa tayari kuzungumza chochote kabla ya kikao hicho lakini akaahidi kuzungumza baada ya kikao kama kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo
Yanga imeweka msimamo wa kutocheza tena mechi hiyo baada ya kutoridhishwa na kitendo kilichofanywa na Bodi ya ligi ambacho ni kinyume na kanuni za uendeshaji wa mpira nchini
Mabingwa hao wa ligi kuu kwa msimu mitatu mfululizo waliandika barua ya kuomba wapewe alama tatu na magoli matatu lakini Bodi ya ligi ilijibu kuwa hawatapewa alama tatu kwa kuwa taratibu za mchezo huo hazikukamilika