Afisa Habari/Msemaji wa zamani wa Yanga Haji Manara ameutaka uongozi wa klabu hiyo kuitisha Mkutano wa dharura wa wanachama kujadili kauli iliyotolewa na Rais wa TFF Wallace Karia juu ya madai ya Yanga baada ya kuahirishwa kwa mchezo dhidi ya Simba kinyume na kanuni
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari jana, Manara alisema kauli alizotoa Karia katika mahojiano na kituo kimoja cha redio zimeidhalilisha Yanga na viongozi wake
Manara amesema Wanayanga wana wajibu wa kudai haki yao na mamlaka ina wajibu wa kutenda haki kwa mujibu wa kanuni lakini inasikitisha kuona wale waliopewa mamlaka ya kuwasikiliza wanatamka lugha za kibabe na kejeli
"Bado mpaka sasa najiuliza kwa nini Rais wa TFF (Karia) ametoa kauli kama zile, sifahamu anataka kutuambia nini"
"Lakini nikisoma na kuangalia lugha ya mwili wake, naona hiki ni kiburi cha madaraka"
"Madaraka yakishakulevya unadhani unaweza kusema jambo lolote, unadhani unaweza kutenda chochote"
"Kusema hiki kinachofanyika ni ujinga na utoto ni dharau, ni ulevi wa madaraka"
"Kusema muende mkacheze Sinema Zetu ni dharau kwani hata hizo Sinema ni eneo kubwa linalonufaisha wasanii wengi. Sinema sio jambo la hovyo kwani linaingiza mapato makubwa kwa nchi. Hata Rais wa nchi kacheza film"
"Nani atatoka kumjibu? nafahamu viongozi wetu ni waoga kwa sababu katengeneza mazingira ukimjibu tu unafungiwa. Lakini viongozi wa Yanga walipaswa kutoa tamko kulaani kauli hizo mara moja baada ya kutamka," alisema Manara