Jumamosi March 08 rekodi nyingine inakwenda kuandikwa katika mechi za watani wa jadi kati ya Yanga dhidi ya Simba
Ni pale timu hizo zitakapoumana katika mchezo wa ligi kuu ya NBC utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa saa 1:15 usiku
Takwimu za jumla zinaiweka Yanga juu zinapokuja mechi za Dabi ya Kariakoo. Haji Manara ambaye amewahi kuwa msemaji wa Yanga ana kauli yake maarufu kuwa hakuna timu imefungwa mara nyingi na Yanga Duniani kuliko Simba
Kudhihirisha hilo katika mechi nne zilizopita, Simba hawajui ushindi unafananaje wanapocheza na Yanga
Bahati mbaya kwa Simba Jumamosi wanakwenda kukutana na Yanga iliyobora zaidi pengine kuliko nyakati yoyote ukitoa ile iliyoshinda mabao 5-1 msimu uliopita
Baada ya kupoteza mechi mbili mbili mfululizo za ligi kuu, Yanga ilijipanga upya, ikimfuta kazi aliyekuwa kocha wake mkuu Miguel Gamondi na kumleta Sead Ramovic 'Germany Machine'
Ramovic alifanya kazi kubwa ya kurejesha utimamu wa wachezaji na licha ya kuanza vibaya michuano ya ligi ya mabingwa, Almanusra Yanga ipindue meza kutinga robo fainali ya michuano hiyo lakini unaweza kusema walikosa bahati katika mchezo wa kuhitimisha hatua ya makundi dhidi ya MC Alger na kulazimishwa suluhu ya bila kufungana katika dimba la Benjamin Mkapa
Hata Ramovic alipoondoka, kocha mpya Miloud Hamdi ameendeleza falsafa ileile, timu yake ikiendelea kufunga mabao kama mvua!
Mwanzoni mwa msimu Yanga haikuwa ikifunga mabao mengi lakini kwa sasa ndio timu inayoongoza kwa kuzifumania nyavu ikifunga mabao 58 kwenye ligi
Takwimu hizo zinakuonyesha Yanga ndio timu yenye safu bora ya ushambuliaji huku utatu wa Clement Mzize, Prince Dube na Stephane Aziz Ki wakihusika katika mabao 44 kati ya 58 yaliyofungwa
Ni wazi itakuwa mechi ngumu hasa ikizingatiwa mazingira ya mchezo huo, matokeo yake yanaweza kuamua hatma ya ubingwa msimu huu
Lakini Yanga inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa ndio timu bora, litabaki jukumu la wachezaji kudhihirisha ubora wao kwa kushinda