Clement Mzize ni jina kubwa kwa sasa kwenye soka la Bongo. Kipaji murua cha kizawa. Kwenye akauti za mitandao za Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kuna picha na video zake likiwamo moja ya mabao yake bora kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika alilolifunga dhidi ya TP Mazembe
Hii ndiyo maana anaimbwa sana. Anatakiwa na kila klabu kutokana na kiwango chake na tayari baadhi zilishatuma ofa mezani. Nini kitatokea. Tusubiri tuone.
Ni mchezaji ambaye Yanga ina kila sababu ya kujivunia mafanikio yake kwani ni mchezaji aliyelelewa Jangwani akianzia timu ya U20
Namba zake kwenye Ligi Kuu Bara si mchezo tangu apandishwe timu ya wakubwa akitokea ile ya vijana na mchezo wake wa kwanza kutambulishwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar Septemba 13, 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kilichofuata ni historia.
Katika mchezo huo, aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Farid Mussa dakika ya 80 Yanga ikiongoza kwa mabao 2-0 na ingawa hakufunga lakini dakika 10 tu alizocheza zilitosha kuandika jina lake kwenye historia ya kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wakibeba taji hilo mara tatu mfululizo.
Hadi sasa Mzize amecheza Yanga kwa misimu mitatu na amefanya makubwa na kusababisha vigogo wa soka Afrika ikiwamo Wydad Casablanca ya Morocco kuisaka saini yake.
Mzize alipandishwa kikosi kikubwa akitokea kile cha pili na aliyekuwa Mkurugenzi wake wa Ufundi, Mwinyi Zahera na Kocha Said Maulid msimu wa 2021/22.
Bao lake la kwanza alifunga dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na katika misimu mitatu aliyocheza amefikisha mechi 70 na kufunga mabao 21 kwenye mechi za Ligi Kuu pekee.
Msimu wake wa kwanza 2022/23 alicheza mechi 20 akifunga mabao matano na kutoa pasi moja ya bao, 2023/24 alicheza mechi 29 akifunga mabao sita na kuasisti saba na msimu huu hasi sasa Yanga ikiwa imecheza mechi 21 na zote akipata nafasi ya kucheza, amefunga mabao 10 na kutoa pasi nne za mabao.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa nyota wengi wanaopandishwa, huwa hawaingii kikosi cha kwanza moja kwa moja na ndivyo ilivyokuwa kwa Mzize na ameruka vihunzi vingi hadi kujihakikishia namba katika vikosi vya makocha tofauti kutokana na ubora wake licha ya kuanza kwa kupata dakika chache za kucheza hadi kuaminiwa