Aliyekuwa Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga Simon Patrick amelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuivunja Kamati ya Waamuzi baada ya mfululizo wa matukio ya waamuzi kufanya makosa yenye shaka ndani yake
Akitoa maoni yake baada ya mchezo kati ya Namungo Fc dhidi ya Simba uliopigwa jana huko Ruangwa, mchezo ulioibua maswali mengi juu ya hatma ya soka la Tanzania, Simon ambaye sasa ni Mwanasheria Msaidizi Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (International Criminal Court), amesema anaamini baadhi ya waamuzi hawafanyi makosa hayo kwa bahati mbaya, bali wanafuata maelekezo
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Simon ameandika ujumbe huu;
"Ukweli usiofichika ni kwamba Yanga na Simba zimekua kubwa na zenye nguvu kuliko mamlaka za soka nchini.
Wasimamizi wa soka letu wako tayari kuzibeba hizi timu ili kuwafurahisha watu kuliko kutenda haki.
Kadri muda unavyosonga, ligi inayoitwa ya nne kwa ubora barani Afrika inazidi kuwa ligi ya vituko kiasi kwamba inakuwa aibu kuisifia mbele ya watu wenye akili.
Waamuzi wa mechi ya leo wamechezesha kwa maelekezo mpaka wao wenyewe wameona aibu kwa vituko walivyofanya.
Waamuzi hawafanyi makosa kwa bahati mbaya kama wengi wanavyodhani, bali wanatekeleza maelekezo waliyopewa.
Muda umefika wa kuvunjwa kwa Kamati ya Waamuzi Tanzania pamoja na waamuzi wote, kwani hawana mchango wala msaada wowote katika maendeleo ya soka la nchi yetu.
Shame on you Waamuzi!"