Kocha Mkuu wa Yanga Sead Ramovic amesema licha ya kuondoshwa katika michuano ya ligi ya mabingwa hawataweka vichwa vyao chini na wataendelea na 'project' ya kujenga Yanga imara zaidi
Jana Yanga ililazimishwa suluhu ya bila ya kufungana dhidi ya MC Alger katika mchezo ambao Wananchi walihitaji ushindi ili kutinga robo fainali
Akizungumza baada ya mchezo huo, Ramovic alisema wameumia kwa kukosa nafasi ya kusonga mbele lakini hawapaswi kukata tamaa na kudhani huu ndio mwisho wa Yanga kwani ndio kama kazi imeanza
"Hayakuwa matokeo mazuri kwa sababu tulipaswa kushinda mchezo huu lakini haikuwa hivyo, tumetolewa mashindanoni"
"Tulitengeneza nafasi tatu au nne za wazi ambazo kama tungekuwa makini tungezitumia kufunga. Lakini niseme mara nyingi sio rahisi kucheza dhidi ya timu aina hii ambayo iko nyuma muda wote"
"Tulichagua kushambulia kupitia upande wa kushoto lakini naweza kusema mipira ya mwisho kwenye krosi haikuwa mizuri"
"Tutafanya tathmini ya kina kuona ni maeneo gani tumefanya vizuri na maeneo gani tumefanya vibaya ili kuboresha zaidi. Hii ni project ambayo tunapaswa kuendelea nayo naamini tutakuwa na timu bora itakayoleta mafanikio makubwa huko mbeleni," alisema Ramovic
Baada ya kuondoshwa katika ligi ya mabingwa, Ramovic anapaswa kuhakikisha kikosi chake kinatetea ubingwa wa ligi kuu pamoja na kombe la FA