Wachezaji wa Yanga wamepambana kwa jasho na damu kuhakikisha wanarejesha matumaini ya kufuzu robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Yanga haikuanza vyema msimu huu ikipoteza mechi mbili za kwanza dhidi ya Al Hilal na MC Alger, matokeo ambayo yaliwakatisha tamaa wengi kuamini safari ya kufuzu robo fainali haitawezekana
Sare na ushindi dhidi ya TP Mazembe, kisha ushindi mwingine dhidi ya Al Hilal jana umefufua matumaini ya kufuzu robo fainali Yanga sasa ikihitaji ushindi katika mechi ya kuhitimisha hatua ya makundi dhidi ya MC Alger itakayopigwa Jumamosi, Januari 18
Hii ni mechi ambayo mashabiki wa Yanga wanapaswa kutumia vyema nafasi yao ya mchezaji wa 12 kwa kujaza dimba la Mkapa
Katika mechi mbili za nyumbani zilizopita, mashabiki hawakujaza uwanja pengine ni kutokana na hali ya kukata tamaa baada ya matokeo yasiyoridhisha katika mechi zilizopita
Lakini wakati huu, katika mechi muhimu ya kuamua hatma ya Yanga kufuzu robo fainali, Wananchi wana kila sababu ya kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono wachezaji wao ambao wamepambana katika nyakati ngumu
Yaani tiketi za mchezo huo zinapaswa kumalizika kabla ya siku ya mchezo ili kupeleka ujumbe kwa wapinzani wao kuwa wanakwenda 'kutaabika' pale Lupaso siku ya Jumamosi
Hii ni mechi ambayo MC Alger wanapaswa kukutana na ugumu pale kwa Mkapa iwe nje au ndani ya uwanja