Beki na nahodha wa Fountain Gate Laurin Makame amebainisha kuwa yuko tayari kutua kwa Wananchi endapo mabingwa hao wa Tanzania Bara watamalizana na waajiri wake
Yanga inatajwa kuwa katika mchakato wa kusajili beki mwingine wa kati mzawa ili kuongeza nguvu katika safu yake ya ulinzi ambayo kwa sasa inawategemea nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Bacca
Makame ambaye pia mara kadhaa ameitwa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' na kuitumikia timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes', ndiye anayeonekana kuwa chaguo sahihi kutua Jangwani kuongeza nguvu
Beki huyo mwenye uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya juu, amesema bado ana mkataba na Fountain Gate lakini haumzuii kujiunga na timu nyingine kama makubakiano yatafikiwa
"Mimi kazi yangu ni kucheza mpira na naweza kucheza timu yoyote kama mkataba utakavyokuwa unanitaka"
"Kwa sasa siwezi kuzungumzia tetesi, ninauachia uongozi wangu na timu husika kufuata utaratibu kwa kuzungumza na waajiri wangu," alisema Makame
Dirisha la usajili lilifunguliwa jana ambapo tayari Yanga imetambulisha usajili wa mlinzi wa pembeni kiraka Israel Mwenda aliyetua kwa mkopo kutoka klabu ya Singida BS
Mwenda anamudu kucheza kama mlinzi wa kulia na kushoto. Katika dirisha hili Yanga pia huenda ikaongeza kiungo mwingine mkabaji na mshambuliaji