Wakati kocha Sead Ramovic akiendelea kupambana kuirudisha Yanga katika ubora wake, uongozi chini ya Rais Injinia Hersi Said umemuhakikishia uungwaji mkono na pengine kuna maamuzi magumu yanaweza kuchukuliwa pale dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa, Jumatatu ijayo, Disemba 16
Baada ya Ramovic kulalamika juu ya fitness ya wachezaji kuwa chini, juzi Yanga ilimtangaza Adnan Behlulovic (43) mtaalam wa mazoezi ya viungo kuongezwa kusimamia eneo la utimamu wa miili ya wachezaji akishirikiana na Taibi Lagrauni
Imeelezwa Ramovic pia ametaka maboresho katika kikosi chake akihitaji kuimarishwa katika baadhi ya maeneo yaliyoonyesha kuwa na mapungufu
Maeneo hayo ni safu ya ulinzi (beki wa kati, kushoto), kiungo mkabaji na mshambuliaji
Safu ya ulinzi upande wa kushoto kwa sasa Yanga inamtegemea zaidi Nickson Kibabage ambaye hata hivyo katika mechi za karibuni ameoneka kuzidiwa na majukumu katika eneo lake
Chadrack Boka amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na kupelekea Yanga kukosa huduma yake katika mechi nyingi muhimu
Yanga ina walinzi watatu tu wa kati, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Bacca. Hivi karibu eneo hilo limekumbwa na changamoto Job akikosa mchezo uliopita dhidi ya MC Alger akiwa majeruhi huku Bacca akiendelea kukosekana katika mechi za ligi kuu akitumikia adhabu ya kadi nyekundu
Bacca amebakisha mchezo mmoja kumaliza adhabu yake. Lakini ni wazi nae amepitia changamoto ya kupoteza umakini wake katika mechi za karibuni pangine kutokana na kutumika mfululizo
Bacca, Job na Mwamnyeto wametumika sana katika misimu hii miwili katika majukumu ya klabu na timu ya Taifa
Eneo la kiungo cha ukabaji Khalid Aucho amekosekana katika mechi nne zilizopita akiwa majeruhi. Kukosekana kwake kunachangia Yanga kukosa utulivu eneo la kiungo
Yanga ilimsajili Aziz Andabwile katika dirisha lililopita kuongeza nguvu katika eneo hilo hata hivyo nae ni majeruhi
Taarifa za kitabibu zimebainisha kuwa Andabwile ambaye Miguel Gamondi pia alimtumia kama mlinzi wa kati, anaweza kukosekana kwa muda mrefu
Safu ya ushambuliaji ni eneo lililozungumzwa zaidi kukosa ufanisi msimu huu licha ya kuwa na washambuliaji kama Prince Dube, Jean Baleke, Clement Mzize na Kennedy Musonda
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya MC Alger Rais wa Yanga Injinia Hersi Said alieleza kutofurahishwa na matokeo ambayo timu yake imeendelea kupata katika michuano ya CAF na kuahidi watafanya kazi na kocha Ramovic ili kuirejesha timu katika ubora wake