Meneja wa Habari na Mawasilino wa Yanga, Ali Kamwe, amesema wanafahamu mechi dhidi ya Al Hilal itakuwa ngumu hivyo amewataka wanachama na mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwaongezea hamasa wachezaji wao
Akiendelea kuwahamasisha mashabiki wa Yanga katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam kujitokeza kwa wingi dimba la Mkapa siku ya Jumanne, Kamwe ameeleza umuhimu wa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwaongezea ari wachezaji
Β "Ni mechi ngumu, lakini kwa ukubwa wetu na umoja wetu, wanachama na mashabiki wakiungana, wakijazana uwanjani kwa kuwashangilia wachezaji wetu, tutaifanya kuwa nyapesi, wachezaji na benchi la ufundi wapo tayari kwa vita hii," alisema Kamwe
Aliongeza wachezaji wao watarajiwa kupambana na kuhakikisha wanampokea kocha mpya kwa ushindi na si matokeo mengine
"Wale waliokuwa katika vikosi vya timu ya taifa tunajua wengi walicheza kwa hiyo bado wana utimamu wa mwili, kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal, kwa maana hiyo haitampa shida sana kocha wetu, kinachotakiwa hapo ni muunganiko tu ili kupate ushindi kwenye mchezo wa kwanza ambao ni muhimu sana," alisema Kamwe
Aliongeza hawana hofu na mchezo huo licha ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara na badala yake wataongeza umakini kuelekea mchezo huo
"Hatuna hofu na mechi hii eti kwa sababu tulipoteza mechi zilizopita, badala yake imetufanya sasa tuwe makini kwenye michezo yote inayofuata, hatutadharau mechi wala hatutaingia uwanjani kwa mazoea," Kamwe alisema