Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema uamuzi wa kumuondoa Kocha Miguel Gamondi umefanyika kwa maslahi mapana ya klabu
Kamwe amesema Kocha Sead Ramovic ameajiriwa na Yanga baada ya kujiridhisha ni mtu sahihi wa kuchukua nafasi iliyoachwa Gamondi
Msemaji huyo wa mabingwa watetezi ligi kuu ya NBC, amesema uongozi hautajibu maoni ya wachambuzi kuhusu kocha huyo mpya lakini majibu yatapatikana uwanjani
"Tunayasikia maoni ya mapendekezo ya wachambuzi katika vyombo vya habari kuhusu kocha wetu, Sead Ramovic, tunawaambie tu hatuna muda wa kujibu, lakini mtayapata majibu uwanjani"
"Wakati tunamsajili kocha Nasreddine Nabi, ilikuwa kama hivi, alitoka kupoteza mechi mbili dhidi ya Simba, akifukuzwa na El Merrikh baada ya miezi mitatu tu. Lakini Nabi ameondoka hapa na medali ya CAF akishinda makombe yote ya ndani"
"Hata kwa Miguel Gamondi ilikuwa hivyo hivyo, wengi walihoji Yanga kumuajiri kocha aliyekaa miezi 6 bila ya kazi baada ya kutimuliwa huko alikokuwa akifanya kazi awali"
"Lakini Gamondi nae ameondoka akiwa na heshima kubwa baada ya kazi nzuri aliyofanya hapa. Kwa hiyo niseme uongozi wa Yanga haufanyi kazi kwa kusikiliza maoni ya wachambuzi, msubiri majibu yenu mtayapa uwanjani," alisema Kamwe
Baada ya kutua jana, Ramovic tayari ameanza majukumu yake ambapo jana usiku alifanya kikao na benchi lake la ufundi kwa ajili ya kuweka sawa program zake za mazoezi katika maandalizi kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Al Hilal utakaopigwa Novemba 26