Ni takribani mwezi mmoja umebaki kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Disemba 16 2024 ambalo litadumu kwa mwezi mmoja na kufungwa Januari 15 2025
Itakuwa nafasi nyingine kwa Yanga kuboresha kikosi. Hivi karibuni Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe alidokeza tayari michakato ya usajili imeanza
Kamwe alifichua mmoja wa wachezaji aliyekuwa katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wake, alikuwepo uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 19 katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0
Imeelezwa Yanga inaweza kuongeza nyota wasiopungua watatu katika dirisha dogo ili kuimarisha kikosi kuhakikisha ubingwa wa ligi kuu unabaki Jangwani kwa msimu wa nne mfululizo na kuongeza nguvu katika ligi ya mabingwa
Maeneo ambayo yataguswa na maboresho hayo ni safu ya ulinzi, kiungo na eneo la safu ya ushambuliaji
Beki wa kati
Yanga inatarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi kwa kusajili beki mwingine wa kati. Kwa sasa Yanga ina mabeki watatu wa kati Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Bacca huku kiungo mkabaji Aziz Andambwile akibadilishiwa majukumu na kutumika kama mlinzi katika baadhi ya mechi
Changamoto ambayo Yanga ilikutana nayo katika mchezo dhidi ya Tabora United baada ya kuwakosa Bacca na Job, imemlazimu Rais wa Yanga Injinia Hersi Said kurudi sokoni kusaka beki mwingine
Kiungo mkabaji
Kwa sasa eneo la kiungo mkabaji, Yanga inamtegemea zaidi Khalid Aucho ambaye mara kadhaa husaidiwa na Salum Abubakar 'Sure Boy' na Jonas Mkude. Ukiangalia wote umri umewatupa mkono na hivyo kuna ulazima wa kuongeza damu changa katika eneo hilo
Kuna uwezekano mkubwa Yanga ikamsajili kiungo mkabaji wa Maniema Onoya Sangana (21) ambaye alikaribia kutua Jangwani katika dirisha lililopita la usajili
Mshambuliaji
Licha ya kuwa na washambuliaji wanne, eneo hilo limekuwa na ufanisi mdogo mpaka sasa msimu huu
Yanga imefunga mabao 14 kwenye ligi, ni mabao manne tu yaliyofungwa na washambuliaji Clement Mzize (2), Jean Baleke (1) na Kennedy Musonda (1)
Kuna uwezekano mkubwa Yanga ikaachana na mshambuliaji mmoja wa kigeni na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji mwingine
Hapa Baleke na Musonda wanaweza kuwa kwenye presha kubwa kwani licha ya kuwa hajafunga kwenye ligi, Prince Dube alipachika mabao manne hatua ya awali michuano ya ligi ya mabingwa