Kwa sasa mashabiki wa Yanga wametega sikio kwa uongozi wao wakisubiri taarifa rasmi juu ya tetesi zinazosambaa mitandaoni kuhusu hatma ya kocha Miguel Gamondi
Juzi baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Tabora United, ilielezwa kuwa mabosi wa Yanga chini ta Rais Injinia Hersi Said walikutana kwa dharura kujadili mwenendo wa timu
Mapema kabla ya mchezo siku hiyo, Kamati ya Utendaji ilikutana katika kikao cha kawaida kwa mujibu wa katiba kujadili masuala mbalimbali ya klabu
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amewataka mashabiki na Wanachama kuwa watulivu kwani si kila taarifa wanaiona mitandaoni wanapaswa kuiamini
Kamwe amesisitiza kitengo chake ndio kina dhamana ya kutoa taarifa yeyote kwa Wanachama
Hata hivyo haitakuwa ajabu kama itatokea uongozi wa Yanga ukaachana na kocha Gamondi licha ya kazi nzuri aliyofanya Jangwani tangu alipotua msimu uliopita
Maisha ya makocha katika klabu za mpira wa miguu hulindwa na matokeo mazuri. Pale inapotokea matokeo sio mazuri, mtu wa kwanza kuwajibishwa ni kocha
Kama uongozi wa Yanga utalazimika kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi ni wazi jambo hilo inapaswa lifanyike haraka kwani ni takribani wiki mbili zimebaki kabla ya mchezo wa kwanza hatua ya makundi ligi ya mabingwa dhidi ya Al Hilal
Lakini kama Gamondi anaendelea basi ni wazi amepewa masharti ya kuhakikisha Yanga haipotezi mchezo huo, kwani kama Yanga itakosa ushindi dhidi ya Al Hilal hakutakuwa na uvumilivu tena