Jana Yanga ilipoteza mechi ya pili mfululizo ligi kuu ya NBC kwa kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Tabora United katika mchezo uliopigwa uwanja wa Azam Complex
Unaweza kusema Tabora United waliokota 'embe dodo' mchangani kwani walicheza na Yanga iliyoonekana kuwa imechoka
Licha ya kumiliki mchezo kwa zaidi ya asilimia 80, Yanga haikutengeneza nafasi nyingi za wazi. Ukiacha mkwaju wa penati ambao Stephane Aziz Ki alikosa, 'on target' ya maana ilipatikana katika dakika ya 94 Clement Mzize akifunga bao la kufutia machozi
Wazungu wana msemo wao, ni siku mbaya kazini na siku kama hii humkuta kila anayefanya kazi
Yanga imekuwa bora sana msimu huu, ikishinda mechi nane mfululizo za ligi kuu bila ya kuruhusu bao kabla ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Azam Fc
Licha ya kupoteza mchezo uliopita, Yanga ilikuwa bora mbele ya Azam tena ikiwa pungufu, lakini jana ikiwa na wachezaji wote 11 haikuwa bora
Haya sio matokeo ya hadhi ya Yanga, hivyo hakuna namna ya kukwepa lawama kwa benchi la ufundi na wachezaji kwani wamepewa dhamana ya kuwapa furaha mashabiki lakini hawajafanya hivyo katika mechi mbili zilizopita
Bado ni mapema sana kuamini Yanga imepoteana baada ya kufungwa mechi mbili. Licha ya vipigo hivyo bado inashika nafasi ya pili tena ikipitwa alama moja tu na wanaoongoza ligi hiyo, Simba
Sasa ni muda wa kurudi uwanja wa mazoezi kwa kocha Miguel Gamondi na vijana wake. Angalau sasa kuna takribani wiki mbili na siku kadhaa kabla ya kucheza mechi nyingine ambayo ni katika ligi ya mabingwa dhidi ya Al Hilal
Vipigo hivi viwe chachu kwa Yanga kurudi ikiwa imara zaidi na kurejesha furaha kwa mashabiki wake