Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mchezo mmoja unatarajiwa kupigwa jijini Dar es salaam
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga watashuka uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuchuana na Tabora United
Ni mchezo muhimu kwa Yanga kwani ushindi utawarejesha kileleni mwa msimamo wa ligi
Yanga imetoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Azam Fc, hivyo Wananchi leo wataingia dimba la Azam Complex wakidhamiria kuwafuta machozi mashabiki wao kwa kushinda mchezo huo
Hata hivyo wanakwenda kukabiliana na Tabora United ambayo imeimarika zaidi ikipata ushindi katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Pamba Jiji na Mashujaa
Washambuliaji Yacouba Songne na Heritier Makambo pengine leo wataiongoza Tabora United dhidi ya waajiri wao wa zamani
Yanga itashuka katika mchezo huo bila ya mabeki wake tegemeo Dickson Job na Ibrahim Bacca wanaotumikia adhabu
Job anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano wakati Bacca atakosa mechi tatu akitumikia adhabu ya kadi nyekundu
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi pia amethibitisha beki Yao Kouassi hatakuwa sehemu ya mchezo huo akiendelea kuimarika kutokana na majeraha aliyopata katika mchezo dhidi ya Coastal Union
Mchezo unatarajiwa kupigwa saa 12 jioni..