Licha ya ubabe inaoendeleza katika soka la ndani, Yanga inaendelea kujiimarisha lengo likiwa kutamba katika anga la Kimataifa pia
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amefichua kuwa watashusha nyota mwingine wa Kimataifa pale dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Disemba 15
Kamwe amesema mazungumzo na mchezaji huyo yako katika hatua za mwisho ambapo alikuwepo uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi iliyopita katika mchezo wa derby ya Kariakoo dhidi ya Simba
"Nataka niwaambie tu Yanga hii bado, Januari kutakuwa na ongezeko la mchezaji mwingine wa kigeni, tunahitaji kuchukuwa ubingwa wa Afrika"
"Huyo mchezaji alikuwepo uwanjani katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo na amekuja kufanya mazungumzo na kusajili tayari kwa kuanza kazi katika michuano ya kimataifa," alisema Kamwe
Msimu huu Yanga imepania kufanya vizuri zaidi katika ligi ya mabingwa ambayo msimu uliopita iliishia hatua ya robo fainali
Wananchi wako kundi A katika makundi wakiwa pamoja na TP Mazembe, Al Hilal na MC Alger
Novemba 25/26 mechi ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya Al Hilal itapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa