Licha ya kuwakosa wachezaji 12 ambao wako kwenye majukumu ya timu za Taifa, kikosi cha Yanga kilirejea mazoezini juzi kujiandaa na mchezo wa dabi huku wakiahidi wataendeleza vipigo kama kawaida
Meneja wa Yanga, Walter Harrison, amesema baada ya mapumziko ya muda mfupi, wachezaji wa timu hiyo ambao hawakuitwa kwenye vikosi vya timu za taifa walirejea mazoezini ili kujiandaa na mchezo huo muhimu
"Tulikuwa na mapumziko mafupi, lakini tumerejea tena na hii ni kwa ajili ya wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kuziwakilisha nchi zao katika michezo ya kimataifa, kila kitu kinaenda vizuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Simba"
"Wachezaji waliobaki wanajiandaa vyema ili wenzao wakirejea wote wawe na utimamu wa mwili, programu hii itawapa wanachama na mashabiki wa Yanga kile ambacho tunakitarajia," alisema Walter
Aidha, Waolteraliwataka mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi kwa sababu kikosi chao kipo imara na wana matumaini ya kuendelea kuwapa furaha kwa kuendeleza kilio kwa wapinzani wao
"Hatujawaambia wachezaji wetu wajilinde wakiwa kwenye timu za taifa ili wasiumie wasije kukosa mchezo dhidi ya Simba, hapana, tunataka wapambane kwenye timu zao kwa sababu wakifanya hivyo pia ni sifa kwa Yanga, na inaongeza wigo wa kutoa wachezaji wengi zaidi siku za mbele"
"Sisi tunaamini watarejea salama salmini na kuwahi kucheza mechi hiyo na nyingine bila ya kupata majeraha," alisema
Yanga kwa siku za karibuni imekuwa mbabe kwa Simba, ikishinda michezo mitatu mfululizo, miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mmoja wa hatua ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii
Mara ya mwisho kukutana ilikuwa ni Agosti 8, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ikishinda bao 1-0
Msimu uliopita wa Ligi Kuu, pia ilipata ushindi michezo yote miwili, ikishinda mabao 5-1, mchezo wa mzunguko wa kwanza na waliporudiana walipata ushindi wa mabao 2-1, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa