Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC utakaopigwa kesho Jumapili katika uwanja wa Azam Complex
Akizungumza katika mkutano na wanahabari mapema leo, Gamondi alisema anatarajia mashabiki wataburudika katika mchezo huo kwani zinakutana timu mbili ambazo hupenda kucheza mpira
Aidha amesema jambo muhimu kwake ni kushinda mchezo huo pasipo kujali wamefunga mabao mangapi
"Tupo vizuri na tuna motisha ya kuelekea mchezo wetu wa kesho dhidi ya KMC timu ambayo inapenda kucheza soka safi kama sisi kwahiyo tunatarajia kuwa na moja ya mechi nzuri sana"
"Tunafahamu hautakuwa mchezo mwepesi kwakuwa wenzetu nao watafanya Jitihada ili wapate ushindi lakini tupo hapa kwaajili ya kupambana na tunaamini tutawaheshimu na tutafanya vizuri"
"Mara zote nasema yaliyopita huwa yamepita, kila mechi huja tofauti. Msimu uliyopita tulicheza nao Chamazi na Morogoro hivyo utakuwa mchezo tofauti japokuwa tuna uzoefu wa kucheza nao na kwangu mimi napenda kufunga magoli mengi na kutengeneza nafasi nyingi lakini sote tunatambua kuwa jambo la muhimu kabisa kesho ni kupata Alama tatu," alisema Gamondi
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, kiungo kiraka Denis Nkane amesema morali ya wachezaji iko juu na jambo muhimu kwao ni kuibuka na ushindi
"Kikubwa sisi wachezaji tunatambua umuhimu wa Alama tatu hivyo kitu cha kwanza tunachokiwaza ni ushindi bila kujali idadi ya magoli lakini tunajua furaha waliyoizoea Wananchi nasi tuna morali ya kuwafurahisha hapo Kesho "
"Maadalizi tuliyoyafanya yanatupa nguvu na imani ya kushinda mchezo wa kesho dhidi ya KMC japokuwa tunatarajia kukutana na ushindani mkubwa lakini tupo imara na tunawaomba Wananchi wajitokeze kwa Wingi Uwanjani ili tushinde pamoja," alisema