Juzi Yanga ilikuwa Ethiopia kuikabili CBE SA katika mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania tiketi ya hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Bao la Prince Dube liliihakikishia Yanga kuondoka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa saa 9 Alasiri
Licha ya ushindi huo maoni ya wadau wengi ni kutofurahishwa na ushindi huo mdogo
Kulikuwa na nafasi nyingi ambazo kama Yanga wangezitumia ipasavyo, Wananchi wangeibuka na ushindi mnono zaidi
Lakini hoja hapa ni Yanga kulaumiwa kwa ushindi mdogo ugenini! Yaani kwa sasa Yanga wameweka 'standard' yao kuwa 'wanaweza kukupasua' katika uwanja wako
Popote ambapo Yanga inacheza, mashabiki wanachotarajia ni ushindi tu, hii ndio tabia ya timu kubwa
Misimu miwili nyuma Yanga ilicheza michuano ya kombe la Shirikisho ambayo walifanikiwa kutinga fainali na kukosa kombe kutokana na kanuni tu kwani mechi yao ya fainali dhidi ya USM Alger ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2, magoli mawili ya ugenini yakawabeba USM Alger
Katika michuano hiyo, Yanga ilishinda mechi zote za ugenini walizocheza katika hatua ya mtoano yaani Club Africain 0-1 Yanga (GS), Rivers United 0-2 (QF) Yanga, Marumo Gallants 1-2 (SF) Yanga na USM Alger 0-1 Yanga (F)
Kwenye makundi walipoteza mechi moja ugenini dhidi ya US Monastrir, wakashinda moja dhidi ya TP Mazembe na kutoka sare moja dhidi ya Real Bamako
Ili uone Yanga kushinda ugenini ni jambo la kawaida kwao angalia matokeo ambayo watani zao Simba wameyapata dhidi ya Al Ahly Tripoli jana
Simba inapongezwa kwa kutoka suluhu ya bila kufungana dhidi ya Al Ahli Tripoli huko Libya katika mchezo wa kombe la Shirikisho wakati Yanga inalaumiwa kwa kushinda 1-0 katika mchezo wa ligi ya mabingwa