Kesho Jumamosi Yanga itashuka dimbani Ethiopia kumenyana na CBE SA katika mchezo wa mkondo wa kwanza raundi ya pili ligi ya mabingwa barani Afrika
Mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Abebe Bikila, jijini Addis unaochukua mashabiki 25,000 walioketi, utaamuliwa na mwamuzi wa kati, Issa SY kutoka Senegal aliyekuwa hapa nchini wikiendi iliyopita katika mchezo wa Tanzania dhidi ya Ethiopia wa kuwania kucheza Fainali za Mataifa Afrika (Afcon) 2025.
SY amewahi kuamua mechi ya Yanga iliposhinda ugenini dhidi ya Club Africain kwa bao 1-0 kisha kufuzu kibabe hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Novemba 9, 2022 pia aliwahi kuwa mezani Oktoba 20, 2023 wakati Simba ikilazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya Al Ahly ya Misri katika African Football League (AFL).
Waamuzi wengine wa mchezo huo wa kesho dhidi ya CBE SA, ni Djibril Camara atakayekuwa mwamuzi wa kwanza msaidizi, Nouha Bangoura atakayekuwa msaidizi wa pili, huku Douda Gueye atakuwa mezani na wote pia wanatokea Senegal, wakati Kamishna wa mchezo ni Michel Gasingwa kutoka Rwanda huku mtathimini wa waamuzi ni Peter Edibe kutoka Nigeria
Yanga ilitua Ethiopia jana na Wananchi leo wanakamilisha maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo utakaopigwa saa 9 Alasiri