Kiungo mshambuliaji wa Yanga Stephane Aziz Ki amesema msimu huu hataki presha ya kuwania ufungaji bora jukumu hilo akiwaachia washambuliaji Prince Dube, Jean Baleke, Kennedy Musonda na Clement Mzize
Aziz Ki anayeichezea Yanga kwa msimu wa tatu, ndiye Mfungaji Bora wa Ligi msimu uliopita akitupia mabao 21 na kabla ya kuja nchini alishawahi kunyakua kiatu kama hicho katika Ligi Kuu ya Ivory Coast akiwa na ASEC Mimosas
Kabla ya Aziz Ki, Mfungaji Bora wa Ligi Kuu alikuwa ni Fiston Mayele aliyekuwa nyota wa Yanga pia kisha kutua Pyramids ya Misri sambamba na Saido Ntibazonkiza aliyekuwa Simba kila mmoja akimaliza na mabao 17
Kiungo mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso, alisema msimu uliopita alikuwa na presha kubwa kutokana na mashabiki wa Yanga walikuwa wanataka kuona anakuwa mfungaji bora, japo haikuwa malengo yake, lakini safari hii hataki tena kuishi maisha hayo na anakabidhi kazi hiyo kwa akina Dube na Jean Baleke
Aziz KI alisema ujio wa washambuliaji hao wapya, yaani Dube na Baleke kumempa utulivu mkubwa kwani anaamini katika uwezo wao kuwa watakwenda kufanya makubwa ukizingatia kuwa kazi yao kubwa ni kufunga na haoni kwa nini Dube asinyakue tuzo hiyo kwa uwezo alionao wa kucheka na nyavu
"Imani yangu ipo kwa Dube, kwani jamaa anastahili kunipokea tuzo hii. Sio siri msimu uliopita nilikuwa na presha kubwa kutokana na mashabiki wa Yanga kutaka kuona nakuwa mfungaji bora mbele ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ niliyekuwa nachuana naye, japo haikuwa shabaha yangu, nilifanikiwa"
"Kwa kikosi tulichonacho mshambuliaji kama Dube ni rahisi kufunga sana, kwani viungo ni wengi ambao wana uwezo mkubwa wa kumlisha mipira hata katika mechi kadhaa zilizopita nadhani mmeona kilichotokea. atafunga," Aziz Ki alinukuliwa na Mwanaspoti
Katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar Dube angeweza kufunga zaidi ya mabao mawili kama angekuwa na utulivu lakini walikuwa ni Maxi Nzengeli na Clement Mzize walioihakikishia Yanga ushindi wa mabao 2-0
Mpaka sasa Dube ameifungia Yanga mabao matano katika mechi mbalimbali kuanzia wakati wa pre-season. Ni mshambuliaji ambaye anaweza kufanya kile anachoamini Aziz Ki