Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Maxi Nzengeli, amesema amefurahia kufunga bao la kwanza la msimu kwa timu yake pamoja na kufikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Wakongomani wenzake, Heritier Makambo na Fiston Mayele
Nzengeli anakuwa Mkongomani watatu kufunga mabao ya kwanza ya msimu kwa Yanga, baada ya kufunga bao la kwanza katika ushindi wa magoli 2-0 ambao waliupata ugenini dhidi ya Kagera Sugar, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera Alhamisi iliyopita
"Nimefurahi sana kwa sababu nimekuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao msimu huu katika kikosi chetu, lakini pia nimeambiwa nimefuata nyayo za Wakongomani wenzangu, kaka zangu, Makambo na Mayele ambao waliwahi kufanya kama mimi, kwa maana hiyo nimeendelea kupeperusha vyema bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo hapa Tanzania," alisema Maxi
Katika mchezo huo, Yanga ilishinda mabao 2-0, goli la pili likiwekwa wavuni na Mtanzania Clement Mzize, dakika mbili kabla ya mechi kumalizika
Msimu wa Ligi Kuu 2018/2019, Makambo alikuwa mchezaji wa kwanza wa Yanga kufunga bao la msimu, akipachika bao katika mechi iliyofanyika Agosti 23, mwaka 2018, timu hiyo ikicheza dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam
Makambo alifunga bao dakika ya 30, mechi iliyoisha kwa Yanga kushinda mabao 2-1, goli la pili likifungwa na beki, Kelvin Yondani kwa mkwaju wa penalti wakati lile la kufutia machozi la Mtibwa Sugar likiwekwa wavuni na Haruna Chanongo
Kwa upande wa Mayele, yeye alifunga bao la kufungulia msimu wa Ligi Kuu 2022/23 katika mechi ambayo Yanga ilicheza dhidi ya Polisi Tanzania, Agosti 16, mwaka 2022 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, mechi hiyo iliisha kwa Yanga kupata ushindi wa mabao 2-1