Kikosi cha Yanga kilichojumuisha wachezaji 20, benchi la ufundi na viongozi kadhaa kimeondoka jijini Dar es salaam mapema leo kuelekea mkoni Kagera tayari kwa mchezo wa ligi kuu ya NBC dhidi ya Kagera Sugar
Mchezo huo utapigwa kesho Alhamisi katika uwanja wa Kaitaba, saa 12:30 jioni
Akizungumza na wanahabari muda mfupi kabla ya kukwea pipa, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema anaiheshimu Kagera Sugar kwani ni moja ya timu zilizoipa Yanga wakati mgumu msimu uliopita
"Kagera Sugar ni mpinzani mgumu, tumekuwa na wakati mgumu kucheza katika uwanja wa Kaitaba pengine ni kwa sababu hatuchezi hapo mara kwa mara"
"Lakini tumefanya maandalizi mazuri na tumejipanga kuhakikisha tunaanza vyema msimu kwa kushinda mchezo wa kwanza," alisema Gamondi
Naye nahodha msaidizi wa Yanga Dickson Job amesema baada ya kufanya vizuri katika mechi dhidi ya Vital'o, wanakwenda Kagera wakiwa na morali kubwa ya kuhakikisha wanashinda mchezo huo
Yanga itafanya mazoezi ya mwisho katika dimba la Kaitaba jioni ya leo tayari kwa mchezo huo