Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amesema Ali Kamwe ataendelea na majukumu yake ya kuwa Meneja wa kitengo cha Habari na Mawasiliano huku wakiendelea kumtafutia nafasi Haji Manara ambaye amemaliza kifungo cha kutojihusisha na soka kwa kipindi cha miaka miwili
Baada ya urejeo wa Haji Manara, kumekuwa na sintofahamu juu ya majukumu yake na Kamwe ambaye aliajiriwa baada ya Manara kufungiwa
"Klabu inamtambua Ally Kamwe kama Afisa Habari kwasababu mpaka sasa mkataba wake unasema hivyo. Haji Manara alikuwa Afisa habari wetu na alifanya kazi nzuri sana katika muda wake na alipopata changamoto akafungiwa kama klabu tulihitaji mtu wa kuisemea klabu na hapo ndipo tulimchukua Kamwe"
"Kwa sasa Kamwe ndie Afisa Habari wetu na upande wa Manara yeye ni Mwanachama wetu na tunaangalia ni sehemu gani ambayo tutamuweka kwenye klabu," alisema Hersi katika kipindi cha Jana na Leo ya Wasafi FM
Hivi karibuni Kamwe alisaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia Yanga baada ya mkataba wa awali kumalizika
Aidha Manara pia alisaini mkataba wa mwaka mmoja na kumfanya awe na mkataba wa miaka miwili ambao utamalizika mwaka 2026