Rais wa Yanga Injinia Hersi Said amesema dhamira yake ya kuhakikisha Yanga inamilika uwanja iko palepale na kwa sasa wanasubiri kukamilika kwa taratibu za Serikali ili waanze mchakato
Hersi alitoa kauli hiyo jana wakati akifanya mahojiano na idhaa ya kiswahili ya Shirika la utangazaji la Uingereza (BBC)
"Tulipeleka ombi kwa Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kuomba kupewa eneo letu la Jangwani pamoja na kuongezewa eneo kidogo ili tuweze kujenga uwanja wetu"
"Katika Mkutano Mkuu uliofanyika mwezi wa sita mwaka huu sote tulimsikia Waziri wetu wa TAMISEMI Mh Mohammed Mchengerwa akithibitisha Serikali imeshatoa eneo hilo na kinachofanyika sasa ni mchakato wa kupata 'documentation' ambazo zitatupa fursa ya kuendelea"
"Tukumbuke eneo lile linabeba mradi mkubwa wa maboresho ya mto Msimbazi liko kwenye mchakato wa Serikali, kuna watu wanalipwa fidia na michakato ya tenda tayari imeanza na karibuni atapatikana mkandarasi ambaye atakuwa sehemu ya mradi huo"
"Nasi tuko katika hatua hizo hizo za kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya sita, pale tutakapokabidhiwa nyaraka nasi tutatoa taarifa rasmi kuhusiana na mkandarasi pamoja na michoro," alisema Hersi
Awali Yanga ilikuwa na mpango wa kujenga uwanja Kigamboni katika eneo walilokabidhiwa na Mkuu wa mkoa wa zamani wa Dar es salaam Mh Paul Makonda hata hivyo baada ya Serikali kukubali ombi la Yanga kuongezewa eneo pale Jangwani ulipokuwepo uwanja wa Kaunda, mpango huo ukabadilishwa
Uongozi wa Yanga unaamini uwanja kujengwa Jangwani ni faida zaidi kwa klabu kwani utavutia uwekezaji na utafikika kwa urahisi na mashabiki