Kiungo mshambuliaji wa Yanga Stephane Aziz Ki amefichua kuwa kabla ya mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam Fc, walimuahidi mshambuliaji Prince Dube kuwa watapambana kwa ajili yake ili kuhakikisha wanashinda Ngao hiyo
Dube alijiunga na Yanga msimu huu akitokea klabu ya Azam Fc ambapo hata hivyo alilazimika kusubiri kwa miezi kadhaa ili uhamisho wake kwenda Yanga ukamilike
"Hii ilikuwa mechi muhimu kwetu, siku zote ni furaha kushinda dhidi ya Azam Fc kwani nao ni timu bora ambayo mara nyingi imetupa upinzani"
"Wakati tunaingia katika mchezo huu tulimwambia Dube (Prince) hii ni mechi yake na kuwa tutapambana ili kuhakikisha tunashinda Ngao hii kwa ajili yake," alisema Aziz Ki
Dube alionyesha kiwango bora katika mchezo ambapo alifunga bao la kusawazisha la Yanga na kuzima ngebe za Feisal Salum aliyetangulia kuifungia Azam Fc bao
Baada ya kuweka mpira kimiani Dube hakuwa na muda wa kushangilia na badala yake akauchukua mpira kuurejesha kati ikiwa ishara ya dhamira ambayo walikuwa nayo wachezaji wa Yanga katika mchezo huo