Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi leo, Uwanja wa Benjamin Mkapa, kushuhudia soka safi litakalochezwa na vijana wake dhidi ya Red Arrows kutoka Zambia katika Kilele cha Wiki ya Mwananchi
Gamondi amesema mchezo wa leo sio wa kusaka pointi wala ushindi kwa ajili ya kombe lolote, hivyo anataka wachezaji wake wafurahie soka, na ushindi utakuja kama wakitandaza soka safi ambalo anataka wacheze
"Ni Siku ya Mwananchi, najua kutakuwa na watu wengi uwanjani, kutafurika mashabiki, najua hili kwa sababu msimu uliopita nilishuhudia pale, lilikuwa ni moja kati ya tukio langu bora sana kuliona, naamini safari hii itakuwa hivyo hivyo, ingawa pia nadhani inawezekana kuna vitu vikaongezeka zaidi kwa sababu tumefanya vyema msimu uliopita," alisema Gamondi
Alisema katika mechi ya leo atajitahidi kuchezesha wachezaji wengi, kila mchezaji apate dakika kadhaa ya kucheza
"Siyo kama naidharau Red Arrows, ni timu nzuri, najua na wao wamekuja kupambana, lakini ukweli unabaki pale pale leo ni burudani zaidi kuliko ushindani, ingawa hii haiwezi kutufanya tusitafute ushindi kwa ajili ya furaha ya mashabiki wetu," alisema
Yanga inakwenda kucheza dhidi ya Red Arrows, ambayo hivi karibuni ilitwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama 'Kagame Cup', michuano ilifanyika nchini Tanzania kwenye viwanja vya KMC, Mwenge na Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam