Kiungo mshambuliaji wa Yanga Skudu Makudubela amesema siri ya mafanikio ya timu hiyo ni malengo ambayo yanawekwa na uongozi lakini presha ya mashabiki ni silaha nyingine inayoifanya Yanga iwe katika ubora wakati wote
Akiwa kwenye msimu wake wa kwanza na Yanga, Skudu amefanikiwa kushinda mataji mawili ligi kuu na kombe la Shirikisho la CRDB pia akiwa sehemu ya kikosi kilichocheza robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Akizungumza katika mahojiano na chombo kimoja cha habari huko Afrika Kusini, Skudu alisema kilichomvutia kujiunga na Yanga ni malengo ya klabu chini ya Rais Injinia Hersi Said
"Wakati najiunga na Yanga nlijua ni kazi gani nakwenda kukabiliana nayo, timu ina malengo makubwa lakini pia ina mashabiki wa kipekee ambao wakati wote wanahitaji kuona timu yao ikishinda"
"Nafurahi kuwa sehemu ya familia na zaidi kuona msimu huu tunawapa furaha mashabiki kwa kushinda mataji mawili," alisema Skudu
Skudu alisajiliwa na Yanga akitokea Marumo Gallants ambapo alikuwa sehemu ya kikosi kilichoiwezesha timu hiyo kucheza nusu fainali ya kombe la Shirikisho la CAF lakini ikatupwa nje kwa kipigo kutoka kwa Yanga
Skudu bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Yanga