Beki wa Yanga, Dickson Job amemwomba radhi Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Hemed Suleiman 'Morocco'
Morocco amekuwa akimwacha Job kwenye kikosi chake tangu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) iliyofanyika Ivory Coast Januari mpaka Februari kwa madai ya utovu wa nidhamu
Morocco alisema wakiwa kwenye mashindano hayo Job aligoma kucheza nafasi ya beki wa kulia kitu alichokitafsiri kama kukosa uzalendo kwa nahodha huyo msaidizi wa Yanga
Kupitia East Africa Redio, Job alikanusha madai hayo yaliyomfanya kuwekwa kando kwenye kikosi cha Taifa Stars na kocha huyo wa zamani wa Namungo na Geita Gold na kusema yeye ni mzalendo na amezitumikia timu zote za taifa katika umri tofauti
Hata hivyo amesema anaamua kumwomba radhi kocha huyo pamoja na Watanzania waliokwazika na madai hayo ya kwamba hana uzalendo kwa taifa lake
"Sijawahi kugomea majukumu ya kocha lakini yeye ni kocha wangu hivyo namwomba radhi pamoja na Watanzania kwani najua walikwazika baada ya kusikia mimi siyo mzalendo," alisema Job