Ligi Kuu ya NBC 2023/24 inahitimishwa leo kwa timu zote 16 kushuka viwanjani
Wananchi Yanga leo wanakwenda kukamilisha ratiba tu katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa uwanja wa Azam Complex
Tayari Yanga imeshakabidhiwa ubingwa waliotwaa wakiwa na mechi tatu mkononi ambapo juzi paredi kubwa la kusherehekea ubingwa huo lilifanyika jijini Dar es salaam
Shauku pekee ilyobaki kwa Wananchi ni kuona kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki anatwaa tuzo ya ufungaji bora
Aziz Ki amepachika mabao 18 akiwa jino kwa jino na Feisal Salum wa Azam Fc mwenye mabao 18 pia
Azam Fc wako ugenini Nyankumbu huko Geita kuchuana na Geita Gold ambayo kimahesabu inaweza kuungana na Mtibwa Sugar kucheza Championship msimu ujao
Geita Gold wanahitaji ushindi dhidi ya Azam Fc kuona kama wanaweza kusogea eneo la play-off na wakati huo huo Azam Fc wanahitaji kushinda kujihakikishia kumaliza nafasi ya pili kuipiku Simba itakayokuwa uwanja wa Benjamin Mkapa kuchuana na JKT Tanzania
Tabora United na Kagera Sugar ziko katika nafasi ya play-off lakini pia JKT Tanzania, Mashujaa, Dodoma Jiji, Singida FG na Namungo Fc zinaweza kuangukia katika eneo hilo kama zitakosa matokeo mazuri katika mechi zao leo hiyo pia ikitegemea matokeo ya timu nyingine
Prisons, KMC, Coastal Union, Simba, Azam Fc na Yanga ndio timu ambazo zina uhakika wa kuendelea kubaki ligi kuu msimu ujao wakati nyingine zitajihakikishia baada ya dakika 90 za mechi za leo