Keshokutwa Jumamosi May 25 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, historia nyingine inakwenda kuandikwa na Yanga
Wananchi wanakwenda kukabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu waliotwaa msimu huu ukiwa ni ubingwa wa 30 katika historia ya Ligi ya Tanzania Bara
Katika kuhakikisha tukio hilo linafana, uongozi wa Yanga umeweka viingilio rafiki kwa kila Mwananchi kumudu
Kiingilio cha chini kabisa Mzunguuko ni Tsh 1,000/- yaani kwa buku lako tu utashuhudia burudani za aina yake ambazo ulipaswa kulipia zaidi ili uzipate nje ya shamrashamra za ubingwa wa Wananchi
Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amewaasa mashabiki kununua tiketi zao mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kama watasubiri siku ya tukio lenyewe
Jumamosi burudani zitaanza mapema tu asubuhi kwa wasanii mbalimbali kutumbuiza kabla ya mchezo dhidi ya Tabora United ambao utafuatiwa na sherehe rasmi za Yanga kukabidhiwa ubingwa
Baada ya Yanga kukabidhiwa kombe lao, Party ya Ubingwa itaanza rasmi, yaani siku hiyo kuna kukesha hapo kwa Mkapa!
Asubuhi ya Jumapili, Wananchi watapata supu kabla ya kuanza parade ya ubingwa kuelekea Makao Makuu ya klabu ya Yanga, Jangwani