Mlinzi wa kushoto wa Yanga Nickson Kibabage amesema afya yake imeimarika na yuko tayari kuendelea na majukumu yake ya kuitumikia Yanga katika mechi zilizosalia kuhitimisha msimu
Juzi Kibabage alipata changamoto ya kiafya katika mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Ihefu Fc ambapo mchezaji huyo alikimbizwa Hospitalini baada ya kupoteza fahamu kutokana na maumivu makali ya kichwa
Kibabage alitibiwa katika Hospitali ya Mount Meru na kuruhusiwa usiku wa siku hiyo hiyo baada ya madaktari kujiridhisha hakuwa katika hatari yoyote
Kibabage amesema ilikuwa mara yake ya kwanza kutokewa na hali hiyo akiwa uwanjani tangu aanze safari ya soka
"Nilizinduka nikiwa hospitali na daktari aliniambia ni hali ya kawaida nisiwe na hofu. Pia walinipatia dawa za kutuliza maumivu na kutundikiwa dripu za maji"
"Nilitoka hospitali saa saba usiku nikiwa mzima kabisa. Kwa sasa niko salama sihisi maumivu yoyote yale na niko tayari kwa michezo ijayo kwani daktari hakuniambia chochote baada ya kuruhusiwa," alisema Kibabage
Yanga ilirejea Dar es salaam jana usiku ambapo baadae leo itaelekea mkoani Dodoma inakokabiliwa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Dodoma Jiji utakaopigwa kesho Jumatano katika uwanja wa Jamhuri