Baada ya kuisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya NBC kwa msimu wa tatu mfululizo, kiungo Stephane Aziz Ki amesema sasa anataka kupambana kuwania tuzo ya ufungaji bora
Jana Aziz Ki pia aliisaidia Yanga kutinga fainali ya kombe la Shirikisho la CRDB akifunga bao pekee la ushindi katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ihefu Fc
Kinara huyo wa mabao katika ligi kuu ya NBC, amesema awali hakuwa akifikiria tuzo binafsi kwani kwake jambo muhimu zaidi ni kuisaidia timu kufikia malengo
"Nikwambie ukweli, mimi sikuwa nafikiria tuzo binafsi, kwangu timu inakuwa mbele kuliko mafanikio binafsi. Nafurahi tumeweza kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu"
"Hili ndio jambo muhimu zaidi kwetu kama timu. Malengo ya timu yamekamilika, sasa ukiniuliza kuhusu kuwania ufungaji bora naweza kukwambia, nitajaribu," alisema Aziz Ki
Aziz Ki amefunga mabao 15 sawa na Feisal Salum wa Azam Fc ambaye pia ana mabao 15. Kila mmoja amesalia na mechi tatu kukamilisha msimu
Kwa kuwa Yanga tayari ni mabingwa, inaweza kuwa rahisi kwa Aziz Ki kupata usaidizi wa wachezaji wenzake ili kuhakikisha anatwaa tuzo hiyo
Sio kwa mashabiki tu, bila shaka hata kwa wachezaji wenzake watapenda kuona Aziz Ki anakuwa mfungaji bora kutoka na mchango wake aliotoa katika mafanikio ya Yanga msimu huu