Licha ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu huku wakiwa na michezo mitatu mkononi, Kocha wa Yanga, Miguel gamondi, amesema kwake bado hawajafikia malengo yao msimu huu mpaka watakapotwaa ubingwa wa kombe la FA
Kocha huyo amewataka wachezaji wake kukumbuka mipango yao tangu walipoanza msimu. Gamondi amesema wanatakiwa kuendelea kupambana na kutwaa ubingwa wa kombe la FA ili kutimiza malengo waliyojiwekea tangu kuanza kwa msimu huu wa 2023/2024
"Bado hatujamaliza msimu, tulikuwa na michuano mitatu, Ligi ya mabingwa, Ligi Kuu na Kombe la FA, kwangu ingawa katika mashindano mawili tumefanikiwa kufikia malengo, bado nahitaji kuona tunachukua kombe la FA," alisema Gamondi
Kocha huyo raia wa Argentina, alisema katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika ingawa walitolewa katika hatua ya robo fainali, walifikia malengo waliyojiwekea kabla ya kuanza michuano hiyo mikubwa Afrika
"Lengo letu kubwa ilikuwa kucheza hatua ya makundi, tulifanikiwa na kwenda mbali zaidi na kucheza robo fainali, ukirudi kwenye Ligi Kuu hivyo hivyo tumefanikiwa kuchukua ubingwa, ukiangalia hapo sasa tumebakisha kombe la FA ambalo nalo lilikuwa kwenye malengo yetu"
Kikosi cha Yanga kilitua Arusha jana tayari kwa mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Ihefu Fc utakaopigwa kesho Jumapili katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid
Mchezo wa kwanza wa nusu fainali kati ya Coastal Union dhidi ya Azam Fc utapigwa leo katika uwanja wa CCM Kirumba