Baada ya kucheza kwa takribani dakika 25 katika mchezo wa kombe la FA, Profesa wa mpira, Pacome Zouzoua leo ataonekana tena uwanjani katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mashujaa Fc ambao utapigwa dimba la Lake Tanganyika
Bila shaka kocha Miguel Gamondi leo atampatia Pacome dakika nyingi zaidi katika mchezo ambao Yanga inazihitaji alama zote tatu ili kusogelea ubingwa karibu zaidi
Pacome ameshiriki kikamilifu maandalizi ya mchezo huo Gamondi akiweka wazi kuwa nyota huyo atakuwa na mchango wake leo
Jana Yanga ilipata mapokezi ya aina yake mkoani Kigoma, Pacome akiwa miongoni mwa wachezaji walioibua shangwe kubwa mbele ya mashabiki
Wananchi waligoma kuondoka katika hoteli ambayo Yanga imefikia hadi pale walipoletewa Pacome na Aziz Ki kuwasalimia
Majira ya saa 10 jioni uwanja wa Lake Tanganyika utafurika Wananchi kushuhudia burudani kutoka kwa timu bora katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati kwa sasa