Baada ya kujihakikishia tiketi ya kucheza nusu fainali ya kombe la Shirikisho la CRDB Bank, kikosi cha Yanga kinahamishia makali yake kwenye ligi kuu ya NBC ambapo siku ya Jumapili May 5 kitashuka uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma kuikabili Mashujaa Fc
Yanga inaendelea na msako wa ubingwa wa 30 ligi kuu ambapo kimahesabu Wananchi wanahitaji alama 11 kutoka mechi sita zilizosalia kumaliza kazi
Alama tatu katika mchezo huo zitawasogeza Wananchi karibu na kukamilisha malengo yao kwani watahitaji kushinda mechi nyingine tatu tu kabla ya kuanza maandalizi ya parade ya ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo
Hata hivyo wanakwenda kuchuana na timu ngumu ya Mashujaa Fc ambayo imeimarika zaidi hasa baada ya maboresho yaliyofanyika katika usajili wa dirisha dogo
Timu hizo zilipokutana katika mchezo wa duru ya kwanza pale uwanja wa Azam Complex, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 Mudathir Yahya akifunga bao la ushindi dakika za jioooooni
Wakati huu Yanga inakwenda Kigoma ikiwa na kikosi chake kamili tofauti na mchezo wa kwanza ambao baadhi ya wachezaji walikosekana kutokana na kuchelewa katika majukumu ya timu za Taifa kwenye michuano ya Afcon 2023 iliyofanyika Ivory Coast