Kiungo mshambuliaji wa Yanga Pacome Zouzoua ameeleza furaha yake baada ya kurejea katika majukumu yake kwenye mchezo wa robo fainali ya kombe la Shirikisho la CRDB Bank dhidi ya Tabora United
Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa Azam Complex jana, ukiishuhudia Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kutinga nusu fainali, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi alimtumia Pacome katika dakika 25 za mwisho
Pacome ambaye kukosekana kwake kuliibua hoja nyingi katika mitandao ya kijamii, amesema alikuwa na shauku kubwa kurejea uwanjani baada ya kukaa nje kwa zaidi ya wiki sita akiuguza majeraha
"Nina furaha kubwa leo, nimerejea tena kuitumikia timu yangu baada ya kukaa nje muda mrefu nikiwa majeruhi"
"Naamini nitaendelea kupewa nafasi zaidi katika mechi zinazofuata lakini jambo kubwa leo ni furaha kuwa katika kikosi kilichoipambania timu na kupata matokeo yaliyotupeleka nusu fainali," alisema Pacome
Akizungumzia urejeo wa Pacome, Mkufunzi wa Yanga Miguel Gamondi amesema kiungo huyo ataendelea kuimarika kadiri anavyoendelea kucheza na anaamini atakuwa msaada mkubwa katika mechi zilizosalia kuhitimisha msimu
"Pacome ni mchezaji mzuri, nafurahi leo ameweza kurejea tena uwanjani, nimempatia takika 20-25, amefanya vizuri"
"Najua sio rahisi kwa mchezaji aliyekuwa majeruhi kwa mrefu kurejea na kucheza katika kiwango cha juu, naamini kadiri atakapokuwa akipatiwa nafasi ataendelea kuimarika"
"Nina hakika atakuwa na mchango katika mechi zilizosalia kumaliza msimu huu," alisema Gamondi