Baada ya kuwasambaratisha watani zao wa jadi Simba Jumamosi iliyopita kwa mabao 2-1, Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo saa 10:00 jioni watashuka kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam kuwavaa Maafande wa JKT Tanzania
Yanga itakuwa na kazi mbili, moja ni kusaka pointi tatu ili kuukaribia Ubingwa wa Tanzania Bara, lakini pia kutaka kuendeleza ubabe ambao iliufanya mechi ya mzunguko wa kwanza
Yanga ilishinda mabao 5-0, mechi iliyochezwa Agosti 29, mwaka jana, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, na kuzima ngebe za msemaji wa klabu hiyo, Masau Bwire, ambaye ameahidi kuwa leo watalipiza kisasi
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema haamini kama wanaweza tena kufunga idadi kubwa ya mabao kama ilivyokuwa mzunguko wa kwanza, kwa sababu anafahamu wapinzani wao watakuja kivingine
"Hakuna mechi rahisi, tunacheza kwa ajili ya kushinda na kutafuta pointi tatu, si kushinda mabao mengi, ikitokea nafasi ya kufunga zaidi tutafanya hivyo"
"Mechi ya kwanza tulishinda mabao 5-0, nakumbuka kuwa tulicheza Azam Complex siyo huku tunakocheza, leo, tunatumia uwanja mwingine, hatufahamu kama utakuwa rafiki, kikubwa sisi tunahitaji pointi tatu tu," alisema Gamondi
Kocha huyo alisema kikosi chake hakikuwa na maandalizi ya kutosha kwa mechi ya leo, tangu walipocheza dhidi ya Simba Jumamosi iliyopita, ila tu wachezaji wake wamefanya mazoezi ya kujiweka sawa