Mshambuliaji wa Yanga Joseph Guede amesema baada ya kupachika mabao katika mechi mbili zilizopita, ataendelea kuzifumania nyavu katika kwenye mechi zilizosalia kuhitimisha msimu huu
Juzi Guede alifunga bao la pili la Yanga katika ushindi wa mabao 2-1 ambao Yanga waliupata dhidi ya watani zao Simba na kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 58
Kabla ya mchezo huo dhidi ya Simba, Guede, raia wa Ivory Coast, aliyewahi pia kukipiga RS Berkane ya Morocco, aliifunga Singida Fountain Gate mabao mawili katika mechi iliyopita
Guede alisema alijiandaa vyema kuelekea mchezo dhidi ya Simba na alimshukuru kocha Miguel Gamondi kwa kumpatia nafasi ya kucheza na kuisaidia Yanga kushinda mchezo huo
"Mimi naamini katika kupambana zaidi hivyo naamini nitaendelea kufunga kadiri kocha atakavyokuwa akinipa nafasi"
"Nimeweza kufunga katika mechi mbili zilizopita, nafikiri ni wakati sahihi kuendeleza juhudi zangu kwa nilipoishia baada ya Simba sasa ni mchezo unaofuata," alisema Guede ambaye pia ana mabao mawili katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) na moja la Ligi ya Mabingwa Afrika
Mchezo unaofuata kwa Yanga ni dhidi ya JKT Tanzania na utapigwa kesho Jumanne katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni jijini Dar es salaam