Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amewaalika watani Simba katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Gamondi amesema anaamini mechi hiyo itakuwa ngumu lakini timu iliyojiandaa vyema itapata matokeo mazuri
Hata hivyo Gamondi amewatahadharisha Simba kuwa wasifikirie kulipa kisasi cha kufungwa bao 5-1 katika mchezo huo kwani Yanga ina kikosi bora na fikra hizo zinaweza kuwagharimu
"Mchezo wa kesho ni mchezo mgumu na tunajua wanataka kuja kucheza ili washinde mechi na kulipa kisasi lakini tumejiandaa kwa hilo, sisi tuna timu imara ambayo inaweza kucheza kwenye presha ya aina yoyote"
"Kama wanadhani wakija na presha ya kulipa kisasi inaweza kuwasaidia basi linaweza pia kuwa kosa"
"Wanapaswa kuja kucheza ili washinde mechi na sio kulipa kisasi kwani timu inapaswa kucheza mchezo ili ishinde na sio kucheza kwa kisasi", alisema Gamondi