Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema wamejiandaa kwenda kusaka ushindi katika mchezo dhidi ya Simba ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo, Gamondi amesema malengo ya kikosi chake ni kushinda mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri katika mbio za ubingwa
"Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huu. Hii ni mechi kubwa sio kwa Tanzania tu bali Afrika nzima"
"Tunajua haitakuwa mechi rahisi lakini jambo muhimu kwetu ni kuhakikisha tunacheza katika mpango wetu"
"Nafahamu matarajio ya mashabiki wetu kuelekea mchezo huu ni makubwa, najua pia sio rahisi kufunga mabao matano katika kila mchezo"
"Tumekuwa na wakati mzuri katika mechi zilizopita, jambo muhimu ni kuendeleza ubora huo ambao tumeonyesha," alisema Gamondi
Gamondi amesema hii ni mechi yao mashabiki, wajitokeze kwa wingi kama walivyofanya katika mechi zilizopita, wawe na timu katika nyakati zote
Ni mechi nyingine ya kuitangaza Ligi ya Tanzania Kimataifa hivyo anaamini itakuwa mechi ya ushindani ambayo itazingatia Fair Play
Kwa upande wa nahodha Msaidizi Dickson Job amesema kama wachezaji wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu na wenye upinzani lakini wamejipanga, watapambana kuhakikisha wanapata ushindi
"Sisi tumejipanga kupambana katika mchezo huu kupata matokeo mazuri. Tunatambua mchezo utakuwa mgumu lakini sisi tumejiandaa kushinda," alisema Job