Joto la mechi ya watani wa jadi linazidi kupanda ambapo wakati Yanga ikiingia kambini Avic Town leo kujiandaa na mchezo huo, watani zao Simba wameelekea Zanzibar
Mapema leo katika mitandao ya kijamii kuliibuka uvumi unaodai kuhojiwa na TAKUKURU kwa kigogo mmoja aliyedaiwa kujaribu kuwashawishi baadhi ya wachezaji wa Yanga kwa fedha ili wacheze chini ya kiwango April 20
Hii ni ishara kuwa mechi ya April 20 itakuwa vita kamili ya soka ndani ya dakika 90 za mchezo huo utakaopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Wakati Simba wakiweka kambi Zanzibar, Yanga haina mpango wa kuondoka Avic Town, maandalizi yatafanyika hapo hapo
Siku hizi Yanga imeachana na ule utamaduni wa zamani kuwa maandalizi ya mechi dhidi ya Simba lazima yafanyike nje ya jiji la Dar es salaam
Jambo la uhakika ni kuwa uongozi wa Yanga utaongeza ulinzi Avic Town ili kuhakikisha wachezaji na benchi la ufundi wanapata utulivu katika maandalizi ya mchezo huo
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesisitizi wanafanya maandalizi huku wakiiheshimu klabu ya Simba licha ya kuifumua mabao 5-1 katika mchezo wa duru ya kwanza
Kamwe amesema wanaamini Simba ina wachezaji bora na wenye uzoefu ambao wamecheza mechi nyingi za derby. Aidha wanatambua timu hiyo ina viongozi makini wanaojua kushinda mechi za aina hii
"Hatuwezi kukaa hapa tukasema eti tunakwenda kumfunga Simba mabao 20, hilo haliwezekani kwani Simba sio mbovu kiasi hicho. Sisi tunajiandaa kwa lengo la kupata ushindi na tunawaomba mashabiki wetu wafahamu hivyo mechi itakuwa ngumu na lazima tupambane ili kushinda"
"Wasiingie katika mtego wa kuaminishwa mchezo huo umekwisha kuwa tayari Yanga tumeshinda. Nafikiri wengi hatujasahau kile kilichotokea katika mechi ya msimu uliopita"
"Mashabiki wanunue tiketi kwa wingi tukaujaze uwanja wa Benjamin Mkapa. Naamini kwa wingi wetu itakuwa motisha nzuri kwa timu kupambana na kuibuka na ushindi katika mchezo huo," alisema