Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amewataka Wanayanga kununua tiketi zao mapema kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba utakaopigwa Jumamosi April 20 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo, Kamwe amesema tangu viingilio vya mchezo huo vilipotangazwa na Bodi ya Ligi juzi, muitikio ni mkubwa
Kamwe amesema hii ni nafasi kwa Wananchi kwenda kuandika rekodi kwa kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa peke yao katika mchezo kama watani zao Simba hawatajitokeza kwa wingi
"Tangu viingilio vitangazwe, muitikio ni mkubwa mpaka sasa tiketi za VIP A zimebaki chache. Tuna jukumu la kuifanya dabi ya Kariakoo iwe kilele cha wiki ya Wananchi"
"Tunataka uwanja wote wa Benjamin Mkapa uwe na rangi za kijani na njano, naamini jambo hili tutalifanya"
"Tunawaomba mnunue tiketi mapema, Taasisi zinazohitaji tiketi kuanzia 50 na wale wanaotoka mikoani wawasiliane nasi kupata tiketi zao mapema," alisema Kamwe
Akizungumzia mchezo husika, Kamwe amesema wanatambua mchezo huo ni mgumu na hivyo wanafanya maandalizi ya kuzingatia ukubwa wa mchezo huo
"Sisi tunaitazama Simba kama timu tishio tofauti na wengi mnavyoitazama. Tunaamini ni timu bora yenye wachezaji wazoefu na viongozi makini ambao wanafamu jinsi ya kupata ushindi katika mechi ngumu"
"Tunaamini Simba ni mpinzani halisi katika mbio za ubingwa hivyo lazima tujiandae kwa tahadhari kubwa"
"Niwatake Wanachama na Mashabiki wetu tujikite katika kuhakikisha timu yetu imepata ushindi. Hatupawi kujadili idadi ya mabao bali tujikite katika malengo ya kupata alama tatu, iwe tumefunga bao moja, mawili muhimu ni alama tatu"
"Najua Wanayanga mnajiamini na mnaiamini timu yenu lakini jambo muhimu tuhakikishe tunajitokeza kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa kuwaongezea hamasa wachezaji wetu," alisema Kamwe
