Wananchi wanahesabu saa kabla ya kuishuhudia timu yao ikishuka uwanja wa Loftus huko Afrika Kusini kuikabili Mamelodi Sundowns katika mchezo wa kuamua timu inayofuzu nusu fainali ligi ya mabingwa Afrika
Kimahesabu bado kila timu ina asilimia 50 za kufuzu baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa Dar kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana
Faida waliyonayo Mamelodi ni kucheza mechi hiyo katika uwanja wao wa nyumbani lakini faida hiyo inakuja na presha kubwa
Presha waliyonayo Mamelodi ni kusaka ushindi katika uwanja wao lakini wakati huohuo kuizuia Yanga isifunge bao
Kama Yanga itafunga bao la ugenini maana yake ni kuwa Mamelodi watalazimika kufunga mabao mawili kwani sare yoyote ya mabao ni faida kwa Yanga
Kwa jinsi mchezo wa kwanza ulivyochezwa Dar, unaona kabisa Yanga wanaweza kupata bao au hata mabao ya ugenini
Bila shaka kocha Miguel Gamondi atatumia mbinu zilezile alizotumia katika mchezo wa kwanza lakini wakati huu ni wazi amewaandaa vijana wake kuwa katili mbele ya lango ya Sundowns
Sio mchezo ambao Yanga itakuwa na mpira kwa muda mwingi lakini hatari yao inatarajiwa kuonekana kupitia mashambulizi ya kushitukiza
Katika mkutano na wanahabari jana Gamondi aliweka wazi kuwa leo mchezaji mmoja kati ya wale waliokuwa majeruhi anaweza kuanza
Kiungo Khalid Aucho huenda akarejea kikosi huku hatma ya Pacome Zouzoua ikitegemea na utayari wake baada ya mazoezi ya mwisho jana jioni
Yao Kouassi hakushiriki mazoezi ya mwisho jana hivyo hatarajiwi kuwa sehemu ya mchezo, upande wake Dickson Job anaweza kutumika kwa mara nyingine
Utakuwa mchezo mgumu lakini kama Yanga watacheza katika ubora waliokuwa nao katika mchezo wa kwanza, lolote linaweza kutokea